Matangazo

ZILIZO KUPITA HIZI HAPA.

Bongo Flava ni sawa na mtoto anayelelewa na mama peke yake

TAARIFA YA HABARI KUTOKA KIBO FM YA TAREHE 04-03-2016

Views:
Video Information
                                TAARIFA YA HABARI MARCH,4,2016.

KWANZA MUKHTASARI WAKE.
- Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro,linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kisangesangeni,wilayani Moshi vijijini,Aboukar Macha,kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.
- Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi Usafiri wa Majini na Nchi Kavu,SUMATRA, mkoani Kilimanjaro,inatarajia kuwafikisha mahakamani madereva na makondakta wanaowatoza abiria nauli kubwa tofauti na zilizopangwa na mamlaka hiyo.

- Polisi nchini Brazil, wanamshikilia kwa mahojiano rais wa zamani wa nchi hiyo, Luiz da Silva, baada ya kuipekua nyumba yake na majengo mengine yanayohusishwa naye, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa kashfa ya ufisadi inayoikabili kampuni kubwa ya mafuta, Petrobras.

HABARI KAMILI.
MOSHI
Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro,linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kisangesangeni,wilayani Moshi vijijini,Aboukar Macha,kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro,Ramadhani Mungi,amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa jana mchana baada ya kupekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na silaha hiyo aina ya Pistol yenye namba ADP 0160A ikiwa na risasi mbili.
Kamanda Mungi amesema mtuhumiwa huyo pia alikutwa na mtutu wa bunduki aina ya Shotgun,akiwa amevificha nyumbani kwake,na amekuwa akivitumia katika matukio ya uhalifu.
Amesema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.
Katika tukio lingine jeshi la polisi limewakamata wakazi wa Msaranga,wikayani Moshi,Philipo John na Sist Philipo,kwa tuhuma za kukutwa na pombe haramu aina ya Gongo lita  40.
Kamanda Mungi amesema watuhumiwa hao pia walikutwa na mitambo mine ya kutengenezea pombe hiyo,ambapo watafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.
DAR ES SALAAM.
Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi Usafiri wa Majini na Nchi Kavu,SUMATRA, mkoani Kilimanjaro,inatarajia kuwafikisha mahakamani madereva na makondakta wanaowatoza abiria nauli kubwa tofauti na zilizopangwa na mamlaka hiyo.

Kaimu Afisa Mfawidhi wa mamlaka hiyo,mkoani Kilimnjaro,Bw.Tadei Mwita,amesema hayo kujibu hoja ya mkazi wa mkoa huo,kuhusu magarina ya daladala zinazosafari kati ya Moshi Mjini na Himo, kuwatoza nauli ya shillingi 1000 abiria wanaoshuka Kiboriloni, Sango Pumuani na Kawawa road, tofauti na nauli iliyopangwa na SUMATRA katika vituo hivyo.  

Mwita amesema kuanzia wiki ijayo wadau wote  watakaoomba leseni kwa ajili ya usafirishaji wa abiria ndani ya mkoa ,watahitajika kuonyesha nauli watakazo toza abiria katika vituo vya katikati kabla ya kufika kituo cha mwisho cha safari zao.

Amesema hivi sasa SUMATRA Mkoa wa Kilimanjaro  imeanzisha utaratibu wa kuwataka wadau wote wanaotarajia kuanza kutoa huduma za usafiri wa daladala, kuonyesha nauli watakazo toza katika vituo vya katikati kabla ya kufika kituo cha mwisho.

MOSHI.

Imeelezwa kuwa utekelezaji wa ahadi ya rais Dk John Magufuli kulinda viwanda vya ndani, imekuwa chachu kwa kiwanda cha sukari TPC wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, na kuwekeza zaidi ya shilingi  bilioni kumi ,kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda hicho.

Afisa mtendaji utawala wa TPC, Jafary Ali ,amesema hayo wakati akizungumzia uzalishaji kiwandani hapo ,wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama mkoani Kilimanjaro iliyotembelea kiwanda hicho.

Ally amesema wanaamini kuwa sukari ya TPC haiuzwi katika mikoa ya kanda ya kaskazini pekee ,na kwamba ipo mifuko maalumu yenye rangi ya njano ambayo inasambwazwa hadi katika mikoa ya Tabora na Shinyanga, huku wafanyabiashara wa Mtwara nao wakihitaji bidhaa hiyo.

Akizungumza na menejimenti ya TPC baada ya kukagua maghala ya kiwanda hicho na yale ya Kahe, mkuu wa mkoa, Amos Makalla aliwahakikishia kwamba serikali itaendelea kuvilinda viwanda vya ndani.

Unaendelea kusikiliza taarifa ya habari kutoka kibo fm,zifuatazo ni habari za kimataifa.
SEOL
Kiongozi wa Korea Kaskazini ,Kim Jong-un ,amevitaka vikosi vya taifa hilo vijiandae kutumia silaha za nyuklia wakati wowote,kuanzia sasa.
Kiongozi huyo amewaambia viongozi wa kijeshi, kwamba North Korea itabadilisha hali yake ya kijeshi, na kuwa tayari hata kutekeleza mashambulio ya kuzuia hatari, shirika la habari la KCNA limesema.
Umoja wa Mataifa umewekea taifa hilo vikwazo vikali zaidi, baada ya Prongyang kufanya majaribio ya nyuklia na makombora ya masafa marefu.
Shirika l habari nchini humo,KCNA,limeripoti kuwa Kim alikuwa akizungumza wakati wa zoezi la kijeshi hapo jana,ambapo inaaminika huo ulikuwa wakati ambao makombora hayo yafyatuliwa.

BRASISLIA.
Polisi nchini Brazil, wanamshikilia kwa mahojiano rais wa zamani wa nchi hiyo, Luiz da Silva, baada ya kuipekua nyumba yake na majengo mengine yanayohusishwa naye, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa kashfa ya ufisadi inayoikabili kampuni kubwa ya mafuta, Petrobras.

Msemaji wa kiongozi huyo ,Jose Crispiniano, amethibitisha kuwa polisi wako kwenye majengo yanayomilikiwa na Silva, ikiwemo nyumba yake na taasisi yake ya misaada wake Silva alizungumza na polisi akiwa kwenye kituo cha polisi kwenye uwanja wa ndege wa Sao Paulo.

Polisi inasema kuhojiwa kwa rais huyo wa zamani aliyejizolea umaarufu wa kuwawakilisha makabwela kwenye uongozi wake, ni sehemu ya uchunguzi wao unaohusisha watu na taasisi nyengine 44 kwenye kashfa maarufu iliyopewa jina la Car Wash, ambapo zaidi ya dola bilioni mbili za Kimarekani zililipwa kwa njia ya rushwa kupata kandarasi za Petrobras. 

JERUSALEM.
Vikosi vya kijeshi vya Israel,vimevunja majengo kadhaa ya Wapalestina, ikiwemo shule moja, kaskazini mwa Ukanda wa Magharibi, na kuziacha familia kumi zikiwa hazina mahala pa kukaa.

Taarifa iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa inasema uvunjwaji huo ulifanyika kwenye kijiji cha Khirbet Tana, kusini mwa mji wa Nablus, ambapo majengo 41 yalivunjwa, na kupelekea Wapalestina 36, miongoni mwao watoto 11, kupoteza makaazi yao.

Hata hivyo, idara ya shughuli za serikali ya Israel kwenye mamlaka ya Palestina, inasema majengo yaliyovunjwa ni 20, ikidai kuwa walitoa tangazo muda mrefu kabla ya uvunjwaji wenyewe.

Israel inakalia asilimia 60 ya kile kinachoitwa Area C, kwenye ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi, ambako ni shida kwa Wapalestina kupata kibali cha ujenzi.
Kabla ya kumaliza taarifa hii ya habari sikiliza tena mukhtsari wake.
- Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro,linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kisangesangeni,wilayani Moshi vijijini,Aboukar Macha,kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria.
- Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi Usafiri wa Majini na Nchi Kavu,SUMATRA, mkoani Kilimanjaro,inatarajia kuwafikisha mahakamani madereva na makondakta wanaowatoza abiria nauli kubwa tofauti na zilizopangwa na mamlaka hiyo.

- Polisi nchini Brazil, wanamshikilia kwa mahojiano rais wa zamani wa nchi hiyo, Luiz da Silva, baada ya kuipekua nyumba yake na majengo mengine yanayohusishwa naye, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa kashfa ya ufisadi inayoikabili kampuni kubwa ya mafuta, Petrobras.
Mwisho wa taarifa ya habari kutoka kibo fm,jiunge nasi tena kesho saa nne kamili kusikiliza kibo fm asubuhi.


Similar Videos