Video Information
UKIFIKA katika mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam utaanza kuhisi kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho ya wengi huanza kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba anayoishi msanii huyo.
Muda wote geti hilo limefungwa. Ili uweze kuingia ndani itakulazimu ubonyeze kengele itakayoashiria kuwa kuna mgeni nje anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi kupenya kirahisi ndani hadi uulizwe shida yako na kama hauna miadi na mtu yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo haitakuwa rahisi kuingia.
Mwandishi awww.sayariblog.blogspot.comlitinga katika nyumba ya msanii huyo na kushuhudia ukimya wa hali ya juu ilhali kuna watu ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na kupokewa na Diamond aliyekuwa ameketi katika sebule iliyonakshiwa na mapambo makini ukutani huku ikiwa na samani chache lakini za gharama kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika mahojiano na Diamond ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na kujibu kwa ufasaha na ufafanuzi mpana.
Mwandishi: Utendaji kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini katika kazi zangu. Mambo yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo yanifikie mimi, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja kwa moja lazima apite huko na hiyo ndiyo staili ya Diamond. Nimejipanga kuhakikisha nafanya kazi gani, kwa wakati gani na sikurupuki tu, japo katika utengenezaji wa nyimbo zangu naweza nikapata wazo basi hapo hapo nikatengeneza mistari.
Mwandishi: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia asubuhi hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi, nikishaamka kitu cha kwanza ni kwenda ‘gym’, mara nyingi ni hapa nyumbani kama unavyoona hapo nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu nyingine zilizopo ndani, mara nyingi hutumia muda wa saa moja. Ifikapo saa sita na nusu huwa naanza kufanya kazi zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo ndio mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo napumzika kwa muda fulani na baadaye jioni huendelea na kazi na mara nyingi kazi zangu huwa nazimaliza usiku wa manane.
Mwandishi: Unalala saa ngapi? Na unalala kwa muda gani?
Diamond: Muda wangu wa kulala mara nyingi ni saa kumi na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi nyingi studio basi nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema kuamka ni saa tano asubuhi ila itategemea na nini ninakifanya siku inayofuata na kama nina kazi maalumu na ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mwandishi: Shughuli gani zinazokuchelewesha mara kwa mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati mwingine shoo. Kwa wiki ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku zote tatu nitalala alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa manane kwa kuwa huwa nakuwa studio na sehemu nyingine ambazo hunilazimu kufanya kazi kwa kipindi kirefu usiku
.
.