Matangazo

ZILIZO KUPITA HIZI HAPA.

Bongo Flava ni sawa na mtoto anayelelewa na mama peke yake

TAARIFA YA HABARI KUTOKA KIBO FM YA TAREHE 23/01/2016

Views:
Video Information
TAARIFA YA HABARI JAN,23,2016.
HII NI TAARIFA YA HABARI KUTOKA KIBO FM.
MIMI NI……………………………..
KWANZA MUKHTASARI WAKE.
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.
- Watu watatu wamefariki dunia,na wengine 35 kujeruhiwa vibaya baàda ya basi walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es salaam kuelekea Morogoro, mali ya kampuni ya bm yenye namba za usajili T916 BQX kuligonga ubavuni lori la mizigo lenye namba T184 CGX na kuangukia kwenye bonde pembeni ya barabara na kupinduka mara nne.
- Polisi nchini Canada wamesema kuwa watu wanne wameuawa katika ufyatulianaji wa risasi katika shule moja katika Mkoa wa Saskachewan, katikati mwa Canada.

HABARI KAMILI.
DODOMA.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.
Ametoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais – Tamisemi kwenye mkutano uliofanyika ofisi ya Tamisemi mjini Dodoma.
Waziri Mkuu ameitaka ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa na kuongeza kuwa jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Pia amesema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia vema.

MOROGORO.
Watu watatu wamefariki dunia,na wengine 35 kujeruhiwa vibaya baàda ya basi walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es salaam kuelekea Morogoro, mali ya kampuni ya bm yenye namba za usajili T916 BQX kuligonga ubavuni lori la mizigo lenye namba T184 CGX na kuangukia kwenye bonde pembeni ya barabara na kupinduka mara nne.

 Kamanda wa polisi mkoa wa morogoro Leonard paul amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi ambalo lilishindwa kupunguza mwendo baada ya lori ambalo lilikua linaovateki lori lililoaribika huku na majeruhi kulalamikia wizi uliofanywa na waliofika eneo la tukio baada ya ajali

Daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro,Francis Semwene amesema watu wawili wamefariki katika eneo la ajali na mmoja amefariki akiwa hospital hapo huku majeruhi wanne kati ya 35 wakiwa kwenye hali mbaya kutokana na kuumia sana ambapo amesema italazimika kuwakata baadhi ya viungo iwapo watashindikana kushonwa.

TANGA.
Mpango wa taifa wa kueneza nishati itokanayo na kinyesi cha wanyama umeelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa maeneo ya vijijini kwani licha ya kuwapatia mbolea bora, bayogesi inawawezesha kupata nishati ya kupikia, kutoa wanga na hata mabaki yatokanayo na uzalishaji bayo gesi kutumika kama dawa dhidi ya mbu na wadudu wengine waharibifu.

Akizungumza katika sherehe ya uzinduzi wa awamu ya pili ya mpango wa kueneza bayogesi nchini katika kijiji cha Boza, wilaya ya Pangani mkoani Tanga hivi karibuni, mmoja wa wanakijiji walio na mtambo wa bayogesi ameelezea anavyonufaika.

Kwa upande wake mratibu wa mpango huo, Lehada Cyprian Shila, amesema tokea wazindue mpango wa uenezi wa bayogesi wa taifa mwaka 2009 wamekwifanikiwa kujenga mitambo ya bayogesi ipatayo 20, 700.

Mpango wa taifa wa kueneza matumizi ya nishati jadidifu ya bayogesi ulianza mwaka2009, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kueneza nishati barani Afrika ulionufaisha mataifa matano yakiwemo Tanzania na Burkina Faso.

ZANZIBAR.

Shule ya msingi ya Kisiwandui iliyopo visiwani Zanzibar, inakabiliwa na uhaba wa vifaa mbalimbali vya kufundishia wanafunzi wasioona na wale wenye ulemavu wa viungo na kuwaomba wafadhili na wasamaria wema kujitokeza na kuwasaidia wanafunzi hao ili waweze kusoma katika mazingira mazuri na kujihisi kama wenzao.

Matatizo hayo yamebainika wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya msaada wa shilingi milioni 20 zilizotolewa na kampuni ya simu ya mkononi ya Zantel kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali vya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya Kisiwandui.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi mfano wa hundi hiyo ya shilingi milioni 20, Mkurugenzi Mkuu wa Zantel Bwana Beneit Janin amesema msaada huo utasaidia kupunguza baadhi ya matatizo yaliyokuwa yakiikabilia shule hiyo na kutoa ahadi kuwa Kampuni yake itaendelea kutoa misaada kwa wanafunzi hao ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi Taifa Khamis Ahmed amesema licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali, wanafunzi hao wamefanikiwa kufanya vyema katika masomo yao na kuendelea katika masomo ya elimu ya juu.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Mwanafunzi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema miongoni mwa matatizo yanayowakabili ni pamoja na ukosefu wa fimbo nyeupe na vifaa vya kuzuia mavumbi kwa wanafunzi wasioona.

Unaendelea kusikiliza taarifa hii ya habari kutoka kibo fm,zifuatazo sasa ni habari za kimataifa.

ADDIS ABABA.
Mabalozi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanafanya mazungumzo kuhusu msukosuko wa Burundi na viongozi wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Mkutano huo unafanywa siku moja baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa kukutana na rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, ambaye uamuzi wake wa kugombea muhula wa tatu wa uongozi ulizusha miezi kadha ya ghasia.
Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, alisema mazungumzo hayo hayakufanikiwa kama alivyotaraji.
Rais Nkurunziza alikataa wito wa mazungumzo, upatanishi na kikosi cha Umoja wa Afrika kuingilia kati.

PORT-AU-PRINCE.
Tume ya uchaguzi nchini Haiti imearisha marudio ya uchaguzi wa urais kwa miaka mitatu sasa, licha ya Rais Michel Martly kutangaza kuwa uchaguzi huo utaendelea.
Tume ya uchaguzi ilisema kuwa ilifanya uamuzi huo kutokana na ukosefu wa usalama.
Kumekuwa na hali ya wasiwasi juu ya marudio ya uchaguzi huo wa Urais, kukiwa na maandamano ambapo makundi ya upinzani yamedai kuwa kuna njama ya kuiba kura.
Rais Martelly anazuiwa katika kugombea Urais huo.
Utawala wake unamalizika kikatiba baada ya majuma matatu na kuna hofu kuwa uchaguzi usipofanywa huenda kukazuka ghasia.
HARARE.
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amerudi nyumbani baada ya likizo ya mwezi mmoja nchi za nje, juma moja baada ya wakuu kukanusha ripoti kwamba alishikwa na ugonjwa wa moyo.
Bwana Mugabe, mwenye umri wa miaka 91, amesema ni mzima kama kigongo.
Anakutana na kiongozi mwengine mkongwe wa Afrika, Teodoro Obiang Nguema wa Equatorial Guinea, ambaye anafanya ziara rasmi nchini Zimbabwe.
Rais Nguema ameongoza Equatorial Guinea kwa miaka 36, mwaka mmoja zaidi ya Rais Mugabe.
OTTAWA.
Polisi nchini Canada wamesema kuwa watu wanne wameuawa katika ufyatulianaji wa risasi katika shule moja katika Mkoa wa Saskachewan, katikati mwa Canada.
Mshukiwa mwanamume ametiwa mbaroni nje ya Shule ya Kijamii ya Loche, ambako kisa hicho kilitokea.
Polisi pia wanaendelea kufanya uchunguzi katika tulio jingine la ufyatulianaji risasi katika kijiji cha watu 3,000 nchini humo.
Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudea, ametaja vifo hivyo kama hofu kubwa inayoweza kumkumba mzazi yeyote.
Mauaji ya watu wengi kwa bunduki nchini Canada si jambo la kawaida , ambako sheria za kuthibiti bunduki ni kali zaidi kuliko Marekani.
Kabla ya kumaliza taarifa hii ya habari sikiliza tena mukhtasari wake.
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.
- Watu watatu wamefariki dunia,na wengine 35 kujeruhiwa vibaya baàda ya basi walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es salaam kuelekea Morogoro, mali ya kampuni ya bm yenye namba za usajili T916 BQX kuligonga ubavuni lori la mizigo lenye namba T184 CGX na kuangukia kwenye bonde pembeni ya barabara na kupinduka mara nne.
- Polisi nchini Canada wamesema kuwa watu wanne wameuawa katika ufyatulianaji wa risasi katika shule moja katika Mkoa wa Saskachewan, katikati mwa Canada.
Mwisho wa taarifa ya habari kutoka kibo fm,jiunge nasi tena kesho saa nne kamili kusikiliza kibo fm asubuhi.








Similar Videos