Video Information
KIRAKA wa Azam FC na Taifa Stars, Shomari
Kapombe, ameweka wazi sababu iliyomfanya aondoke Ufaransa na kurudi
kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine kwa kusema alipokuwa huko kuna
vitu vilipungua katika kiwango chake.
Kapombe amesajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa
miaka mitatu akitokea AS Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la Nne Ufaransa
ambayo ilimnunua kutoka Simba.
Katika mahojiano na Azam TV, Kapombe alisema:
“Napenda kucheza mpira nje ya nchi, lakini kilichonirudisha ni matatizo
yangu na klabu niliyokuwa nacheza kule. Niliposhauriana na washauri
wangu, waliniambia nitafute timu inayonifaa hapa nchini ili niboreshe
kiwango changu.
“Kama unakumbuka niliporudi hapa mambo hayakwenda
sawa kila nilipowasiliana nao kule. Nilipokuwa kule, naona kuna vitu
nilipoteza katika kiwango changu, lakini nashukuru baada ya kuitwa Taifa
Stars nimerudisha kitu na kuwa katika kiwango changu cha kawaida ingawa
siyo sana.”
Kapombe alikwenda mbali na kuweka wazi sababu
iliyomfanya achague kujiunga na Azam akisema anaamini itamsaidia
kukamilisha malengo yake. Pia alisema amevutiwa na klabu hiyo
iliyojitosheleza kwa kuwa na vifaa vyote vya michezo kama uwanja na gym.
“Azam kuna kila kitu, lakini pia nimependa changamoto iliyopo hapa kati ya wachezaji na wachezaji,” alisema.