Video Information
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu,Elizabeth Missokia.
Taasisi ya HakiElimu imekosoa upangaji wa walimu kimikoa kwa kueleza kuwa haukuzingatia mahitaji ya walimu kwenye mikoa husika huku baadhi ya mikoa ikiwa na idadi kubwa kuliko mahitaji na mingine ikiwa na wachache.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia, ugawaji huo haukuzingatia uhaba wa walimu hususani katika mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi.
Alisema mwaka 2013 mikoa ya Arusha, katavi, Morogoro, Pwani, Iringa na Kilimanjaro ndiyo ilikuwa na uwiano mzuri kwa wastani wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 37 ambao tayari walikuwa wamevuka lengo la kitaifa la kuwa na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.
“Mikoa ya Mara, Geita na Tabora ndiyo ilikuwa na uhaba mkubwa wa walimu ambapo wastani wa uwiano ulikuwa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 54… cha kushangaza katika ugawaji wa walimu shule ya msingi walioajiriwa mwaka 2014 mikoa iliyovuka lengo imepewa walimu zaidi,” alisema Missoka.
Alisema katika mikoa hiyo uwiano umekuwa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 34 huku kwenye mikoa mingine ikiwa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.
“Kwa uchambuzi wa HakiElimu tunaona dhahiri kuwa kama walimu 3,733 wangepangwa zaidi kwenye mikoa ya Geita, Mara na Tabota yenye uhaba mkubwa wa walimu kila mkoa ungepata walimu 1,244 na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa walimu kwenye mikoa hiyo hadi kufikia wastani wa mwalimu mmouja kwa wanafunzi 43,” alisema.
Aidha, taasisi hiyo imependekeza serikali kugawa walimu kwa kuzingatia mahitaji kwa kuangalia zaidi mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi, kuhamisha walimu kwenye mikoa iliyo na walimu wengi, kurejesha hadhi ya mwalimu na mafunzo kwa walimu.