Video Information
BEKI wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani na kiungo wa timu hiyo, Athuman Idd ‘Chuji’, wanatarajiwa kuwemo kwenye orodha ya wachezaji watakaoivaa Coastal Union keshokutwa.
Yondani aliumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam, wakati Chuji aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ashanti.
Yanga na Coastal zitaumana keshokutwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara na Daktari wa Yanga, Nassor Matuzya, amesema nyota hao watakuwa fiti kiafya katika mchezo huo.
“Misuli (ya Yondani) ilileta matatizo siku ile alipoumia lakini tulitarajia mechi ya Ashanti angecheza ila bado akawa hajapona vizuri. Sasa hivi tayari ameshapona, yupo safi kabisa, kwa hiyo Jumatatu atakuwa mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo za ligi.
“Kuhusu Chuji, tulimpatia matibabu ya awali tukiwa pale uwanjani, lakini mara baada ya kumpatia tiba hiyo ya awali, tuliona anaimarika haraka na kuweza kutembea vizuri.
“Kutokana na maendeleo hayo, nafikiri kesho (leo) ataweza kufanya mazoezi na wenzake kama kawaida na kama hali yake itazidi kuimarika kama hivi, naweza kumrudisha katika kundi la wachezaji watakaoweza kucheza katika mechi ijayo,” alisema Matuzya.