Video Information
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, leo anahitimisha siku 15 za ziara ya chama hicho ya
kukusanya maoni ya rasimu ya Katiba mpya iliyofanyika nchi nzima,
ukiachilia mbali mikoa ya Lindi na Mtwara ambako Jeshi la Polisi
lilizuia mikutano hiyo. Taarifa ya ofisa habari wa chama hicho, Tumaini
Makene, ilisema kuwa timu ya katibu mkuu leo itahitimisha mabaraza hayo
ya wazi katika wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam. Tangu Agosti 12, mwaka huu, CHADEMA kupitia timu zake mbili za viongozi, wakiongozwa na mwenyekiti na katibu ilianza ziara ya kukusanya maoni ya rasimu ya Katiba mpya kupitia mabaraza ya wazi. Timu ya kwanza iliyoongozwa na Mbowe ilipita katika mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe na kuhitimisha Iringa juzi.
Dk. Slaa na timu yake wao walichanja mbunga katika mikoa ya Tanga,
Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Pwani na Dar es
Salaam na kisha timu hizo mbili zitaungana kuelekea visiwani Zanzibar.
Katika mikutano yao, wananchi mbalimbali waliweza kutoa maoni yao kwa
kuzungumza na kujaza fomu maalumu juu ya mambo wanayotaka yazingatiwe
kwenye Katiba mpya.