Video Information
NDANI ya saa 24 zijazo kitabu kipya cha historia
katika soka kitafunguliwa wakati Gareth Bale atakapotangazwa kuwa
mchezaji ghali zaidi duniani katika uhamisho wa Pauni 94 milioni kutoka
Tottenham kwenda Real Madrid.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Spurs, Franco Baldini,
ametua jijini Madrid tangu juzi Alhamisi kwa ajili ya kukamilisha
uhamisho huo ambao utavunja rekodi iliyowekwa na winga wa Ureno,
Cristiano Ronaldo aliyehamishwa kwa Pauni 80 milioni kutoka Manchester
kwenda Madrid mwaka 2009.
Awali, ofa ya Pauni 85 milioni ya Real Madrid
ilikataliwa mwezi uliopita, kabla ya ofa ya ongezeko la mchezaji mmoja
ambaye ni Fabio Coentrao nalo kukataliwa. Lakini sasa mambo yamenyooka.
Spurs inatazamiwa kupokea kiasi cha Pauni 59
milioni mbele kama malipo ya awali kabla ya kupokea tena kiasi cha Pauni
12 milioni kitakachokwenda kwa mafungu manne kukamilisha dau zima
itakapofika mwaka 2017.
Nyota huyo anatazamiwa kutambulishwa rasmi katika
Uwanja wa Santiago Bernabeu mapema wiki ijayo mbele ya maelfu ya
mashabiki wa timu hiyo ambao wamezoea utamaduni huo kwa miaka nenda
rudi.
Tayari maduka ya Real Madrid yameanza kuuza jezi
ya Bale namba 11 na hata kabla mchezaji huyo hajatambulishwa rasmi,
picha ya jezi yake hiyo ilionekana katika tovuti rasmi ya Real Madrid
tangu Alhamisi usiku.
Kuuzwa kwa Bale kunaweka uwiano mzuri wa hesabu za
Tottenham ambayo mpaka sasa imetumia Pauni 60 milioni kuwanasa mastaa
mbalimbali kwa ajili ya kusaka nafasi ya Top Four.
Tayari imevunja rekodi yake ya uhamisho kwa
kumnasa mshambuliaji wa Valencia, Roberto Soldado, kwa kiasi cha Pauni
26 milioni huku pia ikiwanasa, Nacer Chadli na Paulinho.
Pia kipo mbioni kumnasa mshambuliaji wa AS Roma, Erik Lamela na kiungo wa Anzhi Makachkala, Willian.
Kwa Madrid, hilo litakuwa jibu lao kubwa kwa
Barcelona ambayo katika kipindi hiki cha uhamisho wa wachezaji
ilifanikiwa kuipiga bao Madrid kwa kufanikiwa kuinasa saini ya staa wa
Santos, Neymar kwa kiasi cha Pauni 50 milioni.
Huu ni mwendelezo wa mpango maalumu wa Rais wa
Madrid, Fiorentino Perez, ambaye chini yake mashabiki wa Santiago
Bernabeu wameshuhudia wachezaji wenye majina makubwa kama Zinedine
Zidane, Ronaldo de Lima, David Beckham, Luis Figo na Cristiano Ronaldo
wakitua kuichezea timu hiyo.