Video Information
Kuna mengi ambayo yanatarajiwa kufanyika uwanjani hapo kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa sita usiku. Gazeti hili linakuchambulia burudani kadhaa zitakazokuwepo siku hiyo kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho ‘Abby Cool’.
Simba Vs Yanga (Wabunge)
Imezoeleka kwa jamii kuona wanasiasa wakiwa kwenye majukwaa au bungeni wakipeana changamoto kuhusu hoja mbalimbali, ni nadra kukuta mbunge ‘akijichanganya’ na wananchi wa kawaida mbali na wakati wa kampeni, lakini keshokutwa watajumuika pamoja.
Licha ya kujumuika kwa kucheza na kuimba pamoja, mechi ya soka baina ya wabunge ambao ni mashabiki wa Simba na wenzao wa Yanga, imekuwa ni gumzo kwa kuwa wananchi wengi wanatarajia kuona ushindani wa nguvu.
Zinapokutana katika mechi, Simba na Yanga, hata kama ni mtanange wa kirafiki, miaka yote huwa kuna upinzani mkali, ndiyo maana mechi ya wabunge inatarajiwa kuwa ya upinzani wa juu.
Awali timu hizo zilitifuana mwaka jana ambapo Simba iliibuka na ushindi wa penalti 3-2. Ili kulipa kisasi Abby Cool anasema, Yanga imeongeza wachezaji wa kweli wa kikosi cha sasa cha Yanga ambao ni Ally Mustafa ‘Barthez’, Kelvin Yondani, Athuman Iddi ‘Chuji’ na Mrisho Ngassa.
Simba nayo imejibu mapigo kwa kuwaongeza Amri Kiemba, Said Nassoro ‘Chollo’, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Shomari Kapombe.
Mbunge Athuman Mfutakamba wa Yanga anasema: “Mpaka sasa ni kama tumeshawafunga mabao nane, tunafanya mazoezi kwa siku mara mbili, asubuhi na jioni, yaani tupo fiti balaa.”
Upande wa msemaji wa wabunge wa Simba, Amos Makalla, amesema: “Mashabiki wa Simba wasiogope mbwembwe za Yanga kwa kuwa ni kawaida yao kuongea lakini sisi tupo kivitendo tu akipita mtu mbele yetu tunampiga.”
Mbunge Hamis Kigwangala wa Simba naye anasema: “Wabunge wa Yanga watachezea kichapo siku hiyo, tupo kambini mahali ambapo hapajulikani, tunaogopa fitna, lazima tuwapige tano au sita.”
Abby Cool anaeleza kuwa bingwa wa mechi hiyo atakabidhiwa Kombe la Matumaini ambalo litakuwa likitolewa kila mwaka wakati wa tamasha hilo.
Burudani ya muziki
Rapa Prezzo kutoka Kenya amekuwa akisikika kuwa lazima afanye shoo ya historia kwenye tamasha hilo, lakini upande wa pili, Diamond ambaye kwa sasa yupo juu naye amekuwa akijinadi kuendeleza ubabe wake wa kufunika kwa shoo kali jukwaani.
Diamond anaaminika kuwa staa ambaye yupo juu zaidi kimuziki nchini Tanzania lakini Prezzo amekuwa na bahati ya nyimbo zake kupendwa na Watanzania wengi ndiyo maana hata anapokuwa jukwaani shangwe zimekuwa ni nyingi.
Akizungumzia shoo hiyo, Diamond anasema: “Kati ya matamasha makubwa ambayo nimeyafanya mwaka huu hili ni mojawapo, nafurahia kwa kuwa sehemu ya mapato itaenda kwenye mfuko wa elimu, nitapanda jukwaani na dansa wa kike, namsikitikia huyo Prezzo ataimba nini mbele yangu!”
Juma Nature, Chegge na Temba wote heshima zao zipo juu kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa miaka mingi sasa katika tasnia ya Bongo Fleva, siku hiyo watakuwa jukwaani.
Abby Cool anasema: “Nani ambaye hajui ukali wa hao jamaa! Nyimbo zao ni kali na hata wanapokuwa jukwaani kazi yao huwa mashabiki hawataki washuke.
“Wazee wenzangu pia tumewaandalia burudani kutoka kwa Msondo, Sikinde, lakini watu wa taarabu nao wanakaribishwa kwa kuwa Mzee Yusuf ataiongoza Jahazi Modern Taarab.”
Makongo v Jitegemee
Kutakuwa na mechi ya soka kati ya kombaini ya Makongo Sekondari dhidi ya wenzao wa Jitegemee. Inaeleweka kuwa Jitegemee na Makongo ni shule zenye upinzani wa jadi kimichezo, kwa hiyo siku hiyo bingwa atajulikana na kukabidhiwa kikombe.
Bongo Movie v Bongo Fleva
Mastaa wa filamu, Bongo Movie watakuwa uwanjani kucheza soka dhidi ya wenzao wa muziki, Bongo Fleva.
Mwaka jana katika tamasha hilo timu hizo zilipokutana, Bongo Movie ilishinda kwa bao 1-0, kinachoonekana ni kuwa Bongo Fleva wanataka kurejesha heshima yao.
Nahodha wa Bongo Fleva, H.Baba anasema: “Tunawaonea huruma kwanza wana tabia ya kukodi majeshi kwa kuwa hawajiamini, tupo kambini tunapiga matizi. Tutavaa fulana za Ngwea na Langa ili kuwaenzi wenzetu hao walitangulia mbele ya haki.”
Upande wa staa wa Bongo Movie, JB anasema: “Kwanza nimesikitika sana kumkosa Azzan katika masumbwi, nilitaka kuchapana naye, tatizo ni uzito, nilijiandaa hasa kumchakaza. Upande wa soka mimi ni kocha mchezaji, hivyo nitaanzia benchi.
“Tutacheza mpira wa pasi na tutatumia mfumo wa 3-5-2, tunawaheshimu wenzetu lakini watusamehe kwa kuwa tumeshafanya kikao hao tutawapiga mabao 4-0.”
Viingilio
Abby Cool anasema: “Viingilio vya tamasha hilo, VIP ni shilingi 20,000, VIP B & C ni shilingi 10,000 na mzunguko ni shilingi 5,000.
“Tiketi zinapatikana Zizzou Fashion (Sinza Afrika Sana), Nkiniepa Sports Wear (Tegeta), TSN Supermarket (Mikocheni), TSN Supermarket (Bamaga), TSN Supermarket (Upanga), Samaki-Samaki (Mlimani City), Steers (Kijitonyama), Dar Live (Mbagala), Biggy Respect Big Bon (Kariakoo), Salamanda Bookshop (Posta Opp. Sapna na Oilcom Supermarket (Ubungo).
Usalama wa hali ya juu
“Ulinzi na usalama utakuwa ni wa kiwango cha juu, kutakuwa na askari wa jeshi la polisi, farasi, mbwa, maninja wasiopungua 60 na mabaunsa zaidi ya 50, hivyo watu waje na familia zao kwa kuwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa shoo kila kitu kitakuwa salama.”
Source:Global Publisher