Video Information
AMA hakika duniani kuna mambo! Na lisemwalo
lipo kama halipo basi laja. Ni jambo ambalo ni vigumu kuliamini lakini
ukweli wa mambo ni kwamba limetokea mjini Kahama, Mkoa wa Shinyanga,
kiasi cha kuleta mtafaruku kwa jamii. Ni baada ya vikongwe viwili
vinavyosadikiwa ni vichawi kunusurika kuuawa na wananchi wenye hasira
kali kufuatia kudondoka kutoka angani. Tukio hili la aina yake ambalo
mbali na kustaajabisha limeleta hofu kwa baadhi ya wakazi mjini Kahama,
lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 3 mwaka huu katikati ya Kata za
Majengo na Mhongolo zilizo katika Halmashauri ya Mji wa Kahama. Vikongwe
hivyo vilikutwa vikiwa taabani huku vikiwa vimetapakaa kinyesi.
Vikongwe hivyo, Mwajuma Samaka Mponi (70)
mkazi wa kijiji cha Nduku katika Kata ya Kinaga na Shija Nkwabi (80)
mkazi wa kijiji cha Nyashimbi pia mkazi wa Kata ya Mhongolo katika
Halmashauri ya Mji wa Kahama, vilikumbwa na dhoruba la kudondoka baada
ya kugongana na wanga wenzao wengine watatu waliokuwa katika shughuli
zao angani.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mhongolo,
Emmanuel Kalolo, anasimulia kuwa vikongwe hivyo vilionekana vikiwa hoi
havijitambui vikiwa vimelala ambapo kimoja kilikuwa eneo la Kindi’s Bar
katika barabara ya kwenda Mhongolo huku mwingine akiwa mtaa wa Bariadi
karibu na Café Latino. Kalolo alisema kuwa Waendesha bodaboda (pikipiki)
walianza kumshuhudia kikongwe Mwajuma Mponi tangu alfajiri lakini
hawakumjali kwa kudhani kuwa huenda ni mlevi ama mwendawazimu. Hali
iliendelea hivyo hadi alipotokea mtu mmoja ambaye aliingiwa na mashaka
baada ya kumwona akiwa uchi wa mnyama tena akiwa ametapakaa kinyesi.
Msamaria huyo, Kulwa Samson, kwa jina maarufu’ KR’ ambaye ni Meneja wa
Café Latino, baada ya kumuona bibi huyo aliamua kumpatia msaada kwa
kumuombea nguo katika nyumba za jirani. Samson alisema alibaini hilo
wakati kienda Mhongolo kufuatilia kreti za bia.
Baada ya kumsaidia, bibi huyo alimweleza
kuwa kuna mwenzake mtaa wa pili. Walipomfuatilia walimkuta akiwa
amezingirwa na watu waliokuwa wamemshangaa. Baada pia ya kumsitiri
alimchukua hadi kwa mwenzake na kuwafanyia mpango wa chakula. Baada ya
huduma hiyo aliwakabidhi kwa Kamanda wa Wanawake Kata ya Majengo,
Kuluthum Bujiku, ambapo walianza kuwasaili chanzo cha kuwa katika madhia
hayo. Nao bila kupepesa macho, vikongwe hivyo vilidai vilidondoka
vikiwa katika shughuli zao za kawaida za kila siku usiku. Mashuhuda hao
walisema kuwa vikongwe hivyo vilidai vilikuwa vikitoka katika makao yao
ya shughuli zao huko Nduku wakiwa na wenzao watano wakielekea Dodoma
kuhitimisha kilele cha sherehe za Pasaka. Walisema wakiwa angani
walipata ajali ya kugongana na wenzao waliokuwa wakitoka eneo jingine
hivyo wakajikuta wamedondoka ardhini. Vikongwe hao vilieleza kuwa safari
yao ya Dodoma ilikuwa ya kwenda na kurudi usiku huohuo mara baada ya
kukamilika kwa tafrija yao hiyo ya Pasaka.
Kwa bahati mbaya, walidai, wakiwa njiani
kuelekea Dodoma walikumbwa na dhoruba hiyo na kudai baada ya kugongwa
“pikipiki” yao iliishiwa mafuta. Walisema kuwa wenzao watatu ambao
waliishawahi kukumbwa na dhoruba hiyo mara nyingi, walitoweka katika
mazingira ya kutatanisha na kuwaacha wao wakitapatapa. Waliongeza
kwamba shughuli hiyo ya usangoma imewafikisha maeneo mbalimbali hapa
nchini na walikuwa hawajawahi kudondoka. Baada ya maelezo hayo ambayo
waliyatoa huku kukiwa na umati wa watu ambao walitaharuki na kutaka
kuwashushia kipigo, sangoma hao walinusurika baada ya Samson kuwa tayari
amewapigia simu polisi ambao hawakufanya ajizi kufika eneo la tukio na
kuwakuta watu wenye hasira wakiwa wamejipanga kuwatoa uhai vikongwe hao.
Watu hao walipandishwa katika karandinga huku kikongwe Mwajuma akigoma
kuachia kifuko cheusi alichokuwa amekishika mkono wa kulia ambacho
alidai ni hazina yao muhimu. Vilevile, gari la oolisi lilipata wakati
mgumu kuondoka hapo kwani lilionekana kama vile gurudumu zake zinataka
kuzama ardhini bila sababu. Polisi wilayani Kahama imethibitisha kuwa
inawashikilia watu hao.
Story Na Mwandishi ,Kahama wa GLOBALPUBLISHERS