Video Information
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa dola
milioni 131 zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya chakula, maji na
mahitajio mengine ya dharura huko Zimbabwe katika mwaka huu wa 2013.
Alain Noudehou, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Mwakilishi Mkazi wa
UNDP nchini Zimbabwe ameyasema hayo huko Harare mji mkuu wa nchi hiyo
hapo jana. Noudehou amesema hali ya kibinadamu imeimarika kwa kiwango
fulani huko Zimbabwe ikilinganishwa na mwaka uliopita, suala ambalo
limepelekea kupungua kwa msaada ulioombwa mwaka jana kwa ajili ya nchi
hiyo na kuwa chini ya dola milioni 197. Uzalishaji wa chakula ulipungua
kwa kiasi kikubwa huko Zimbabwe tangu mwaka 2011 kutokana na kuyumba
kwa hali ya kiuchumi na kisiasa. Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na
Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Zimbabwe amesema dola milioni 110 kati
ya msaada wote wa dola milioni 131 ulioombwa zitatumika kwa ajili ya
kuwahudumia watu milioni 1.6 wanaokabiliwa na upungufu wa chakula huko
Zimbabwe.