Video Information
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Uganda zimeunga mkono pendekezo la
vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, la kupelekwa kwa ndege za
uchunguzi zisizo na rubani katika mpaka wa mashariki mwa Kongo.
Umoja wa Mataifa unasema uasi wa miezi tisa uliyoirudisha nchi hiyo
yenye utajiri wa madini katika vita, unaungwa mkono na nchi za Rwanda na
Uganda, madai ambayo yanakanushwa na serikali za nchi zote mbili.Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende alisema serikali yake inakaribisha mpango huo. Mende ambaye pia ni waziri wa mawasiliano aliwaambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kuwa matumizi ya ndege hizo yatavisaidia vikosi vya kimataifa kuboresha usimamizi wa mpaka wenye matatizo unaozitenganisha Kongo na Rwanda.
Kampala ambayo ni mwenyeji wa mazungumzo kati ya serikali ya Kongo na waasi licha ya madai kuwa inawafadhili waasi, iliunga pendekezo hilo kwa tahadhari kwa masharti kwamba ndege hizo hazitumiki katika mashambulizi. Waziri wa ulinzi wa Uganda Chrispus Kiyonga alisema kama ndege hizo zitatumika kwa uchunguzi na kuheshimu uhuru, hilo litakuwa sawa.
Kwa upande wake, Rwanda ambayo ina kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema inaupinga mpango huo hadi pale utakapofanyiwa tathmini. Naibu balozi wa Rwanda katika umoja huo alionya kuwa Afrika isigeuzwe kuwa maabara ya vifaa vya uchunguzi kutoka mataifa ya kigeni.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilisema mwaka uliyopita kuwa Rwanda ilituma vifaa na wanajeshi kupitia milima inayozitenganisha nchi hizo mbili kwa lengo la kuwasaidia waasi wa M23, ambao ilisema wanapokea amri kutoka kwa maafisa wa ngazi za juu nchini Rwanda, akiwemo waziri wa ulinzi. Rwanda ilikanusha vikali ripoti hiyo na badala yake, ikaigeuzia kibao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa kushindwa kuwamaliza waasi wa Rwanda waliyoko nchini humo.
Kundi linalodhibitiwa na Watutsi la M23, ambalo lilipewa jina lake kutokana na makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009, yaliyopelekea waasi wa zamani kuingizwa katika jeshi la Kongo, lilianzisha tena uasi kwa madai kuwa serikali imeshindwa kuheshimu makubaliano hayo. Baadaye lilipanua madai yake na kutishia kusonga mbele kuiangusha serikali ya Rais Joseph Kabila.
Viongozi wa M23 wametangaza katika hatua ya upande mmoja ya kusitisha mapigano siku ya Jumanne, kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo na serikali mjini Kampala, hatua ambayo imeongeza matumaini ya suluhu ya muafaka kukomesha uasi huo.