Video Information
KIBO FM ADHUHURI. 10/12/2015.
MIMI..............
Rais mstaafu wa
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema katika uongozi wake wa miaka 10, hakuwahi
kuagiza mtu asamehewe kontena lake lisilipe kodi na angefanya hivyo, mapato ya Serikali
yasingeongezeka kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.
Akizungumza baada ya
kuwashitukiza wananchi wa Chalinze katika soko kuu la eneo hilo kwa kuungana
nao kufanya usafi kuitikia agizo la Rais John Magufuli jana asubuhi, Kikwete alisema
katika uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu anayestahili kulipa kodi asilipe kodi.
Amesema wakati huu
ambao amepumzika baada ya kustaafu, amepata nafasi ya kusoma mitandao na
magazeti mbalimbali na kukuta baadhi ya watu, wakimshutumu na kumtukana yeye na
familia yake wakimhusisha na ukwepaji kodi.
Kikwete amewataka
Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli katika jitihada anazofanya za
kukabiliana na wakwepa kodi, huku akitoa mfano akisema wakwepa kodi kwa
Serikali ni kama inzi na kidonda, hawaondoki bila kufukuzwa na ukiacha
kuwafukuza wanarudi.
Pia amesema uamuzi
wa Rais Magufuli wa kutumia maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru, kuwataka wananchi
wote wafanye usafi, ni wa busara na si wa kukurupuka kwa kuwa mwaka huu taifa
lilikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu.
.................................................
Wamiliki na
mawakala wa usafiri wa mabasi yaendayo mikoani wameonywa kutopandisha nauli
katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka na watakaobainika
watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kufungwa jela.
Onyo hilo
limetolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna
Msaidizi Mohammed Mpinga wakati wa uzinduzi wa huduma mpya kwa abiria wa
bodaboda kwa njia ya simu ya ‘Fasta Fasta Service’ ambayo itamwezesha abiria
kupata huduma hiyo kwa kufuatwa mahali alipo.
Kamanda Mpinga
amesema imekuwa ni tabia ya wamiliki wa usafiri wa mabasi hayo pamoja na
mawakala wao kuongeza nauli hizo kinyume cha sheria na taratibu zilizowekwa
jambo ambalo linawaumiza wananchi.
Amesema Polisi
Kikosi cha Barabarani kimejipanga nchi nzima ili kuhakikisha wanakomesha
vitendo hivyo na si tu kwa Kituo cha Ubungo pia kwa kupandikiza abiria
watakaokuwa na kazi ya kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika.
..................................................
Rais wa Argentina aliyemaliza
muda wake , Cristina Fernandez de Kirchner, amewaaga maelfu ya wafuasi wake
ambao walikusanyika katikati mwa mji wa Buenos Aires.
Katika hotuba yake ambayo ilijaa hisia nje ya ikulu,
Fernandez alivishutumu vyombo vya habari vya nchi hiyo kwa kuipiga vita
serikali yake ya mrengo wa kushoto.
Fernandez na mume wake ambae tayari ameaga dunia, Nestor
Kirchner, wamekuwa madarakani kwa muda wa miaka kumi na mbili.
Ametetea hali ya uchumi, na kusema hakuna katika utawala
uliopita ambao uliiacha Argentina bila madeni.
Na kuwataka raia wa Argentia kutetea haki zao na maslahi
yao ambayo wameyapata.
Makundi yaliyokusanyika katika eneo hilo yalikuwa
yakiimba wakati Fernandezi akipanda katika jukwaa.
................................................
Mwanaharakati wa haki za binadamu Leyla Yunus ameachiliwa
huru Jumatano wiki hii na vyombo vya sheria vya Azerbaijani kwa sababu za
kiafya baada zaidi ya mwaka mmoja akiwa jela, huku nchi nyingi za magharibi na
mashirika yasio ya kiserikali wakitoa wito wa kuachiliwa kwake.
Mahakama ya Rufaa ya Baku imepunguza hukumu ya miaka
minane na nusu jela dhidi ya Leyla Yunus hadi miaka mitano, ikitetea uamuzi
wake kwamba hali ya afya ya mwanaharakati huyo, ambaye anasumbuliwa na ini na
ugonjwa wa kisukari, imeendelea kuzorota.
Bi Yunus, mwenye umri wa miaka 59, alikamatwa na kuwekwa
rumandekwa muda akiwa na mumewe Arif katika majira ya joto 2014 kwa kosa la
usaliti na ukwepaji wa kodi, tuhuma ambazo wanandoa hao wamekanusha.
Mwisho wa kibo
fm adhuhuri,jiunge nasi tena ifikapo saa kumi kamili kusikiliza kibo fm
alasiri.