Video Information

BAADHI ya
wanaharakati wamevitaka vyombo vinavyotunga sheria nchini kwa pamoja
kwa kushirikiana na wanaharakati kuhakikisha wanashinikiza kutungwa kwa
sheria itakayo simamia bajeti za kila mwaka na pale ambapo Serikali na
idara fulani zinaonekana kukwamisha utekelezaji sheria ichukue mkondo
wake.
Kauli
hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na baadhi ya wawakilishi kutoka
asasi anuai za kiraia ambao walishiriki katika mjadala wa wazi wa kudai
uwajibikaji kwa watunga sera kwa kuzingatia mgawanyo wa rasilimali
kijinsia ulioandaliwa na TGNP Mtandao.
Akizungumza
katika majadiliano mwakilishi wa wa asasi ya Network for Vulnerables
Rescue Foundation (NVRF), Ezekiel William alisema anakerwa na kitendo
cha serikali kupanga bajeti kila mwaka lakini asilimia kubwa ya fedha za
bajeti hasa zile za maendeleo hazipelekwi katika wizara na idara kama
ilivyopangwa.
“…Mimi ni
miongoni mwa watu wanaokerwa na kitendo cha Serikali kupanga bajeti na
bunge kuidhinisha lakini baadaye unasikia idara na wizara zikilalamika
kuwa asilimia 45 ya bajeti ya bajeti zao haikupelekwa hivyo
haikutekelezwa hadi muda unaisha…mwaka mwingine inatengwa nyingine na
mambo ni yaleyale,” alisema William.
“...Kuna
haja ya kutungwa sheria ya kusimamia bajeti, yaani endapo bajeti
haijatekelezwa sheria ichukuwe mkondo wake…washtakiwe wale waliokwamisha
utekelezaji wa bajeti hiyo hii itakuwa ni fundisho na itachochea
maendeleo,” alisisitiza William.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SIKIKA, Irenei Kiria akiwasilisha
mada juu ya huduma zinazotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
changamoto zake, alisema bado sekta hiyo inachangamoto nyingi kwani
uhaha wa vitendea kazi wataalamu katika maeneo mbalimbali ya wizara ni
takribani asilimia 50 licha ya bajeti ndogo inayopangwa kila mwaka.
Naye
Ofisa Miradi wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Bi. Asha
Komba akiwasilisha mada yake juu ya rushwa ya ngono nchini‘Sextortion’
alisema matokeo ya rushwa hiyo yamekuwa na madhara makubwa kiutendaji
jambo ambalo alishauri asasi mbalimbali kuungana kukabiliana nayo kwa
kuhamasisha utoaji taarifa.
Alisema
rushwa ya ngono imekwamisha utendaji kazi na usimamizi maeneo mbalimbali
ndani ya Serikali na nje katika asasi na taasisi anuai jambo ambalo
linakwamisha maendeleo nchini na unyanyasaji wa kijinsia.
Aidha
alisema kuongezeka kwa rushwa za ngono zimeongeza migogoro katika
familia na kuathiri maendeleo ya elimu katika ngazi zote za elimu, pia
alitolea mfano kwamba kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaofeli
kunachangiwa na rushwa za ngono. “…Rushwa za ngono zimeongeza mimba
utotoni, zimechangia kushuka kwa viwango vya elimu na sasa ni kikwazo
katika elimu ya vyuo,” alisema Bi. Komba.
Aliyekuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya ambaye aliongoza mjadala huo
ulioshirikisha asasi anuai kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani
ikiwemo Pwani na Morogoro, aliwataka washiriki kuhakikisha wanaunganisha
nguvu zao na kupaza sauti kusimamia hoja za msingi wanazo ziibua kwa
manufaa ya jamii kwa kuzingatia makundi yote.