Video Information

Akionekana mwenye afya njema, Sheikh Ponda anayetetewa na wakili Batheromeo Tharimo, alifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi licha ya kutokuwepo umati mkubwa wa wafuasi wake.
Mara baada ya kufikishwa mahakamani hapo, wakili Tharimo alidai kuwa amewasiliana na wakili mwenzake, Juma Nassoro, ambaye naye anamtetea Sheikh Ponda, na kwamba kuna ombi waliliwasilisha Mahakama Kuu la kutaka shauri hilo kutoendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Katika ufafanuzi wake juu ya madai hayo, wakili Tharimo alisema kuwa ombi hilo linatokana na rufaa namba 98 ya mwaka 2013 waliyoikata Mahakama Kuu inayohusu Mahakama ya Kisutu kwa shitaka la kwanza la kutotii amri halali ya Mahakama ya Kisutu linalomkabili mshitakiwa huyo mahakamani hapo.
Wakili huyo ambaye alidai kuwa uendeshaji wa kesi hiyo hautaendelea hadi uamuzi wa rufaa waliyoikata Mahakama Kuu utakapotolewa, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutaja kesi hiyo.
Hata hivyo, uliibuka ubishani wa kisheria kati ya wakili Tharimo na wakili wa serikali, Sunday Hiela aliyedai kuna kumbukumbu zinaonyesha kuwa Sheikh Ponda alimkana wakili Tharimo.