Video Information

Waziri Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kupanda kwa bei za aina zote za mafuta za jumla na rejareja, kulinganisha na zile zilizotangazwa Machi 5, mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alitangaza bei hizo jana na kusema zilianza kutumika nchini kote juzi.
Alisema katika mabadiliko hayo, bei ya rejareja kwa petroli imepanda kwa Sh. 11, sawa na asilimia 0.48, wakati ile ya dizeli imepanda kwa Sh. 109 (asilimia 5.36) na bei ya mafuta imepanda Sh. 11 (asilimia 0.50) kwa lita.
Pia alisema bei ya jumla kwa petroli imepanda kwa Sh. 10.67 (asilimia 0.51) wakati ile ya dizeli imepanda kwa Sh. 109.20 (asilimia 5.63) na ile ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh. 11.04 (asilimia 0.57) kwa lita.
“Mabadiliko haya yametokana na mabadiliko ya bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya marekani,” alisema Ngamlagosi
Alisema kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.
Pia, alisema Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta na kwamba, taarifa hizo zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.