Wabunge wawili nchini Libya
walipigwa risasi na kuumizwa
baada ya kundi la waandamanaji
kuwashambulia bungeni katika mji
mkuu wa Tripoli.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema
kuwa wawili hao walipigwa risasi
walipojaribu kutoroka kutoka katika
eneo hilo.
Waandamanaji hao waliokuwa na
ghadhabu walilishambulia bunge
hilo, huku wakitaka bunge lifungwe
na tarehe mpya ya uchaguzi wa
mapema itangazwe.
Kumekuwa na mawimbi ya
maandamano nchini humo kutokana
na uamuzi wa bunge la nchi hiyo
kuhairisha tarehe ya uchaguzi hadi
baadaye mwakani.
Waliolishambulia bunge siku ya
Jumapili walisema kuwa
walighadhabishwa pia na “kutekwa
nyara” kwa waandamanaji waliokuwa
na kikao nje ya bunge.
Walisema kuwa waliohusika na
utekaji nyara huo walikuwa chini ya
uongozi wa waasi wanaotumikia
amri ya bunge.
Waandamanaji hao ambao wengi
wao ni vijana walijihami kwa visu na
vijiti,wakalishambulia bunge huku
wakiwa na ujumbe kwa wabunge
kwa kuimba “jiuzulu,jiuzulu”, kwa
mujibu wa taarifa ya ashirika la
habari la AFP.
Bunge la nchi ya Libya
limeshambuliwa mara kadhaa kwa
zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Nuri Abu Sahmein ambaye ni spika
wa bunge hilo aliambia kituo cha
televisheni cha Al-Nabaa kuwa
maandamano yaliyokuwa ya amani,
yalivurugwa na watu waliojihami.
"Wabunge wawili walipigwa risasi
pale walipojaribu kutoweka mahali
hapo kwa kutumia magari yao,”
alisema.
Haikuwezakana kubaini papo hapo
idadi ya wabunge walioumia.
Picha zilizotumwa kwenye mitandao
ya kijamii zinaonyesha
waandamanaji wakivuta kile
kilichokusudiwa kuwa kiti cha Spika
wa bunge hilo nje ya bunge na
kukichoma.
Mwandishi wa BBC Rana Jawad
ambaye yuko Tripoli anasema kuwa
bunge la Libya limeshambuliwa
mara kadhaa na makundi tofauti,
yakiwemo makundi ya waasi katika
kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Uchaguzi uliokuwa wa amani
ulifanywa na nchi ya Libya katika
mwezi wa Julai mwaka jana, ila
bado nchi hiyo ya kaskazini mwa
Afrika ingali inang’ang’ana kupata
utulivu, miaka mitatu baadaye
tangu kufurushwa kutoka
maamlakani kwa aliyekuwa rais,
hayati Muammar Gaddafi.
WABUNGE WA LIBYA WASHAMBULIWA.
Views:
Video Information