Video Information

Tatizo la ajira ni kubwa hapa nchini, huku wengi wa wahitimu wakionekana kuendelea kuwa mizigo kwa familia zao kwa maana kwamba badala ya kuondoa kero za kiuchumi kwa kupata ajira, wameendelea kuwa tegemezi kwa kukosa kazi za kufanya.
Wapo wazazi maskini ambao walijitahidi kwa kadri wanavyoweza ikiwamo kuuza nyumba au hata kukopa ili wawasomeshe watoto wao wakiamini watakapohitimu wangeweza kuwa na nguvu binafsi kiuchumi, kwa vile wangeajiriwa au wangejiajiri, kwa bahati mbaya si wote ambao wamepata ajira au wameweza kujiajiri.
Zaidi ya watu milioni 197 sawa na asilimia 5.9 ya nguvu kazi duniani hawana ajira, kati ya hao vijana ni milioni 73.8 sawa na asilimia 12.6.
Hali ni mbaya nchini, kwani hata taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Tanzania, watu wengi hawana furaha katika maisha yao; wanaishi tu ilimradi. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni inayoonyesha Hali ya Furaha Duniani (World Happiness Report 2013), imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa wananchi wake kutokuwa na furaha duniani, kati ya nchi 156 zilizofanyiwa utafiti huo. Ripoti hiyo iliandaliwa na kundi la wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa (UN).
Baadhi ya Watanzania wanaamini kinachotakiwa kifanyike nchini ni kuimarisha elimu ya ujasiriamali kwa watu wote ili waweze kujianzishia mambo yao, badala ya kutegemea ajira kama ambavyo wahitimu wengi wa vyuo na shule nchini wanafanya.
"Hali kwa ujumla ni mbaya nchini, wengi hawana kazi, tumeanzisha taasisi iitwayo Sasho Business Solution. Mkakati hasa ni kuwasaidia Watanzania waweze kujiajiri, tuko kwenye harakati za kuomba ufadhili ili kukamilisha tunachotaka kukifanya," anasema Said A. Said, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi iitwayo Sasho Business Solution
Mkurugenzi huyo anasema tayari wameshaendesha mafunzo ya wazi kwa vijana mbalimbali Tanga na Arusha, huku mikakati sasa ikiwa ni kujikita kutoa elimu hiyo katika shule za sekondari an vyuo. "Tumeanza mawasiliano na baadhi ya walimu wa shule za sekondari, tunashukuru kwamba wametupokea vizuri, tunajipanga kuhakikisha tunatoa elimu imara ya namna ya kuanzisha na kuendeleza biashara, pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama vile vyakula vya mifugo ikiwamo kuku, sabuni, mishumaa nakadhalika. Kwa mfano kuku wanalipa sana, ndani ya mwezi tu kuku wanakua...mfano ndani ya mwezi ukawakuza kuku 3,000, kila mmoja ukamuuza Sh7,000, maana yake unapata Sh21 milioni...hata ukitoa gharama za matunzo, bado siyo rahisi ukakosa Sh10,000,000 kwa mwezi," anasema mtaalamu huyo.
Rekodi za Serikali zinaonyesha Watanzania wasio na ajira ni zaidi ya asilimia 11. Tatizo la ukosefu wa ajira ni kubwa zaidi katika jiji kama la Dar es Salaam ambalo takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 31.4 ya wakazi wake hawana ajira. Katika miji mingine ukosefu wa ajira ni asilimia 16.3. Kadhalika takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake wasio na ajira ni kubwa kuzidi ile ya wanaume katika maeneo ya mijini.
"Tumeanzia Dar es Salaam, lakini lengo letu ni kwenda Tanzania nzima, tutakwenda popote tutakapoalikwa," anasema Said.
Shosha ni taasisi ya vijana wasomi waliohitimu vyuo mbalimbali, wameungana kwa lengo la kuangalia namna gani wanaweza kufanya ili kuwasaidia Watanzania wengine kupambana na tatizo la ajira.