Video Information

Padri Mwang’amba (aliye tumbo wazi) akizungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (kushoto).
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa Padri wa Kanisa
Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Mwang’amba ni
mwendelezo wa uhalifu huo ambao Serikali imeshindwa kabisa kuudhibiti.
Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea, Padri
Mwang’amba anasema alikuwa nje ya duka linalotoa huduma za mawasiliano
ya mtandao (Sun Shine Internet Caffee) liliopo eneo la Mlandege Wilaya
ya Mjini Unguja, ndipo alipotokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati Padri huyo akieleza hayo, Rais wa Zanzibar
Dk Ali Mohamed Shein, ameijia juu polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio
ya viongozi wa dini na Serikali visiwani humo, kushambuliwa kwa
kumwagiwa tindikali huku akilitaka kuwakamata waliohusika na tukio hilo.
Kiongozi huyo wa dini, aliyejeruhiwa maeneo ya
usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo
alisafirishwa jana na ndege ya kukodi ya Shirika la Coastal kutoka
visiwani humo hadi Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.
Kwa upande wake, Padri wa Parokia ya Mtakatifu
Joseph, Zanzibar, Thomas Assenga aliyefuatana na kiongozi huyo mpaka
MNH, alisema siku za nyuma Padri Mwang’amba alitolewa vitisho na mtu
ambaye hamfahamu wakati akienda kutoa huduma katika kituo cha wazee cha
Welezo.
Alisema kabla ya kufika kituoni hapo, kuna eneo
ambalo nyakati za asubuhi watu hufanya mazoezi barabarani ambapo kuna
mtu mmoja alimtolea maneno ya vitisho.
Tukio hilo linafuatia tukio la Agosti 7, mwaka huu
ambapo raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18)
walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar na vijana
wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki aina ya Vespa.
Waingereza hao walisafirishwa siku tatu baadaye kurudi kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu.
Utetezi wa Serikali
Siku tano baada ya tukio la Waingereza hao
kumwagiwa tindikali, Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi
iliwataka wananchi kuisaidia kuwafichua na kutoa ushahidi wa uhalifu huo
kwani ni vigumu kuwabaini wahusika.
Kauli hiyo ilitolewa kwa pamoja jana na Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa
Samwel Manyele na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) Eliezer
Feleshi, katika mkutano wao na waandishi wa habari, uliolenga kueleza
mikakati ya kupambana na matumizi yasiyo sahihi ya tindikali nchini.