Video Information

Baadhi ya Watanzania wamekuwa wadaiwa kuuawa na polisi, hakuna tume zinazoundwa.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe (Chadema), jana aliitaka Serikali itoe tamko iwapo
inasubiri hadi polisi waue watoto wao au baadhi ya mawaziri ndipo waunde
tume huru ya kuchunguza.
Mbowe alihoji hatua hiyo bungeni mjini hapa jana wakati alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
Katika swali la nyongeza jana bungeni, Mbowe
ambaye ni Mbunge wa Hai alihoji ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi
cha kuunda tume huru ya kimahakama ili waweze kuchunguza na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria wale wote wanaohusika na mauaji hayo.
“Baada ya kuhoji jambo hili jana (juzi), naibu
waziri alijibu kwa lugha nyepesi sana tena ya kejeli kwamba Serikali
haijaona umuhimu wa kufanya jambo hilo ……..mh, Naibu Spika, raia
wanauawa na Polisi kwa idadi kubwa na wanaendelea kuuawa kila siku
je,mnasubiri hadi watoto wenu wauawe au mawaziri ndipo muone umuhimu
huo,” aliuliza Mbowe.
Katika swali la msingi mbunge wa Mbeya Mjini
Joseph Mbilinyi (Chadema), alitaka maelezo ya Serikali juu jeshi la
polisi kuhusika na mauaji ya mwanafunzi wa Sekondari ya Iyunga, Michael
Sikupya ambalo lilithibitishwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa
Mbeya.
Pia mbunge huyo alitaka kujua ni hatua gani
zilichukuliwa kwa mauaji hayo, na Serikali inasemaje kuhusu kulipa fidia
Familia ya Mzee Sikupya ambaye ni baba mzazi wa marehemu aliyehangaika
na suala hilo zaidi ya miaka 10 bila msaada wowote.
Marehemu Michael Sikupya alikufa akiwa hospitali
mnamo Desemba 3, 2000 saa 5.20 asubuhi akitokea Kituo cha Polisi ambako
alifikishwa yeye na wenzake 53 kwa kosa la kuhusika na vurugu za
kuchoma nyumba ya mwalimu mmoja, Novemba 26, 2000.