Video Information
KOCHA Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, amekubali matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, lakini akalitaja Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa ndiyo chanzo cha matokeo hayo.
Kauli hiyo ya Kibadeni, inakuja wakati ambao Simba ilianza Ligi Kuu Bara kwa sare hiyo ya juzi katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kibadeni alisema awali alikuwa ameiandaa timu yake tayari kwa kupata ushindi katika mchezo huo, lakini mara baada ya kupata taarifa kutoka TFF kuwa baadhi ya nyota hawataruhusiwa kucheza mchezo huo, alilazimika kubadili sura ya kikosi chake.
Kibadeni alisema awali alikuwa amewajumuisha wachezaji wake wapya, mshambuliaji Khamis Tambwe na beki Kaze Gilbert katika kikosi chake lakini akalazimika kuwaondoa kufuatia TFF kueleza kuwa, nyota hao walikuwa hawajakamilishiwa taratibu za uhamisho, wakitokea Vital’O ya Burundi.
“Tulipata taarifa ya kutowatumia baadhi ya wachezaji kutoka TFF majira ya saa sita mchana, ilitusumbua kwa kuwa tayari tulishamaliza upangaji wa timu ya kuanza ambayo naamini ingefanya vizuri katika mchezo wa jana (juzi),” alisema Kibadeni na kuongeza:
“Ukiangalia kwa makini muda ambao tumepata taarifa hizo, ni lazima hali ile ilituathiri kidogo kuanza kufikiria nani tumjumuishe baada ya kuondolewa kwa hao wengine, lakini niseme kwamba hakuna haja ya kutoa visingizio vingi, tutajipanga tayari kwa mchezo ujao.