Matangazo

ZILIZO KUPITA HIZI HAPA.

Bongo Flava ni sawa na mtoto anayelelewa na mama peke yake

Boban na Nyoso waitikisa yanga

Views:
Video Information
KAMA kuna timu yenye mikwara kwenye Ligi Kuu ya Bara hiyo ni Coastal Union. Ipo Dar es Salaam, kesho Jumatano inacheza na Yanga wakati Simba ikikipiga na JKT Oljoro mjini Arusha.
Coastal imeanza msimu na jeuri ya fedha kwa kuwasajili wachezaji wengi wa maana akiwemo Haruna Moshi Boban na Juma Nyosso ambao watanogesha mechi ya kesho huku mabeki na mastraika wa Yanga wakijipanga kisawasawa kuwakabili.
Yanga inajivunia kikosi imara jambo ambalo Coastal haitaki kusikia na utamu zaidi utaanzia kwa mabeki wa kati, Juma Nyosso na Marcus Ndaheli ambao ni wababe kwenye himaya yao, wana nguvu na uzoefu wa kukabiliana na mastraika, Mrundi Didier Kavumbagu na Jerry Tegete wenye uchu wa mabao.
Yanga inasifika kuwa na safu imara ya ulinzi chini ya Mnyarwanda Mbuyu Twite na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa sababu Kelvin Yondani ‘Vidic’ bado hajawa fiti.
Lakini kumbuka kuwa, Coastal ina straika hatari aliyezichapa Simba na Yanga mabao mawili mawili kila mmoja alipokuja na kikosi chake cha URA ya Uganda kwenye mechi za kirafiki, Yoyo Kato raia wa Uganda ambaye ataungana na Kenneth Masumbuko.
Ukija kwenye viungo ndiyo usiseme kwani wote wababe. Yanga itamkosa, Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye ni majeruhi lakini yupo Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, Frank Domayo na Salum Telela ambao nao ni mafundi.
Lakini Coastal nayo ina viungo kama Wakenya, Jerry Santo, Crispin Odulla na Haruna Moshi ‘Boban’ wanaotumia akili zaidi na wanawafahamu vizuri wachezaji wa Yanga kwa uzuri na mapungufu yao.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts alisema: “Tumejiandaa vizuri na tuko tayari kwa mchezo huo, kama unavyojua Yanga inataka kushinda kila mechi iliyo mbele yake ili kutetea ubingwa. Kiufundi tuko sawa.”
Naye Hemed Moroco, Kocha wa Coastal Union alisema: “Naifahamu Yanga kwa uzuri na mapungufu yao lakini sitayaweka wazi kwani jukumu langu ni kuyafanyia kazi mwenyewe ili mambo yaende vizuri.”
Mechi nyingine inayoangaliwa kwa jicho la umakini ni Simba na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Azam FC dhidi ya Rhino ya Tabora Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.
Simba inayonolewa na Abdallah Kibadeni ‘Mputa’ ilitoa sare ya 2-2 na Rhino ya Tabora na katika mchezo huo, haikuwatumia wachezaji wake wa Kimataifa kutoka Burundi ambao ni straika, Amis Tambwe na beki wa kati, Gilbert Kaze kutokana na tatizo la Cheti cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) lakini sasa kila kitu kimekamilika na wataivaa Oljoro.
Wachezaji hao raia wa Burundi wameonyesha morali ya aina yake mazoezini jambo ambalo limempa kiburi Kibadeni na kutamka kwamba amepata watu wa kazi.
Similar Videos