Video Information
Nabil al-Arabi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
amesisitiza kwamba, amani ya kweli haiwezi kupatikana katika Mashariki
ya Kati pasina ya kuundwa nchi huru ya Palestina. Nabil al-Arabi amesema
hayo baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Mashauri
ya Kigeni wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na wenzao wa Umoja wa Ulaya na
kusema kuwa, kadhia ya Palestina ndio iliyokuwa ajenda kuu ya kikao
hicho na kwamba, pande mbili zimesisitiza juu ya kutatuliwa haraka
hitilafu baina ya Palestina na Israel. Mbali na kadhia ya Palestina,
kikao hicho kilijadili pia masuala mengine tofauti kama mahusiano ya
kisiasa, kijamii na kiuchumi. Jamii ya kimataifa imetangaza mara kadhaa
wa kadhaa kwamba, maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu na utawala
wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 yanapaswa kuondoka katika makucha ya
wavamizi wa Kizayuni na kwamba, madhali jeshi la Israel lingaliko katika
maeneo hayo na nchi huru ya Palestina haijaundwa, basi Mashariki ya
Kati, katu haiwezi kunusisha harufu ya amani na utulivu. Imepita miaka
20 sasa tangu yalipoanza mazungumzo yanayojulikana kwa jina la
mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati, huku kukiwa hakuna ahadi
yoyote ile ya Marekani inayojifanya mpatanishi na mbunifu wa mazungumzo
hayo ambayo imetekelezwa; na mazungumzo hayo yameendelea kubakia bila
natija. Mwezi Novemba mwaka 1991 Marekani iliwaita kwa mara ya kwanza
katika meza ya mazungumzo Wapalestina na jamii ya Waarabu kwa ahadi ya
kutekeleza maazimio mawili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo hayo yalikuwa ya kwanza tangu kukaliwa kwa mabavu Palestina.
Kwa mujibu wa vipengee vya maazimio hayo, jeshi la Israel linapaswa
kuondoka bila masharti yoyote katika ardhi inazozikalia kwa mabavu tangu
mwaka 1967 na ardhi hizo kurejeshewa wamiliki wa asili na hivyo kuandaa
uwanja wa kuundwa nchi ya Palestina. Aidha inaelezwa katika vipengee
vya mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati kuwa, nchi ya Palestina mji
mkuu wake ukiwa Baytul Muqaddas inapaswa kuundwa mwaka 1999 baada ya
kuondoka jeshi la Israel kuondoka ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan,
Ukanda wa Gaza na sehemu ya Baytul Muqaddas. Hata hivyo hadi leo sio tu
kwamba, jeshi la Israel halijaondoka katika ardhi za Wapalestina, bali
Tel Aviv hata imeongeza kasi katika kujenga na kupanua vitongoji vya
walowezi wa Kizayuni hali ambayo imeondoa fursa ya kubakia ardhi kwa
ajili ya kuundwa nchi ya Palestina baada ya kupita miaka 65 ya uvamizi,
ukimbikizi na kubakia bila nyumba wananchi wa Palestina. Upanuzi wa
vitongoji vya walowezi wa ni mlolongo wa mzingiro dhidi ya ardhi za
Palestina ambao umekuwa na mbinyo kiasi kwamba, ardhi za Palestina
zimegawanywa na kuwa vipande vipande. Ni miongo 6 sasa ambapo eneo la
Mashariki ya Kati limekuwa likishuhudia vita na machafuko huku chimbuko
la hayo yote ukiwa ni uvamizi na siasa za kupenda kujitanua za utawala
wa kimabavu wa Israel. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Nabil
al-Arabi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu akasema kuwa, ili
kulifanya eneo la Mashariki ya Kati lipate amani na utulivu wa kweli
kuna haja ya kuandaliwa mikakati mipya ya mazungumzo na lengo la
mazungumzo hayo liwe ni kuhitimishwa uvamizi wa Israel.