Video Information
Mashambulio ya anga ya jeshi la
Ufaransa katika ngome za waasi kaskazini mwa Mali licha ya kuwa,
mwanzoni yalishabikiwa na viongozi wa Paris, lakini habari
zinazoripotiwa hivi sasa zinaonyesha kuwa, viongozi wa Ikulu ya Elysee
wameingiwa na kihoro kutokana na tishio la kulipiza kisasi lililotolewa
na al-Qaeda na wanamgambo wanaofungamana na mtandao huo. Rais Francois
Hollande wa Ufaransa amesema kuwa, serikali yake imechukua hatua za
kuimarisha usalama katika maeneo ya watu wengi ikihofia mashambulio ya
kulipiza kisasi kutokana na kuingia kijeshi kaskazini mwa Mali. Kwa
hakika wasiwasi wa Rais Hollande sio wa bure; kwani mmoja wa wasemaji wa
al-Qaeda kaskazini mwa Afrika ametoa indhari kwa Ufaransa na kuitaka
itazame upya uamuzi wake wa kushiriki katika operesheni ya kijeshi dhidi
ya waasi wa Mali. Abou Dardar mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati
ya Tawhidi na Jihadi Magharibi mwa Afrika (MUJAO) ameitahadharisha
Ufaransa na kusema kuwa, ijiandae kukabiliwa na mashambulio ya kulipiza
kisasi ya wapiganaji wao. Hata Manuel Valls, Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Ufaransa amesisitiza kwamba, hali ya sasa nchini Mali inaweza kuandaa
uwanja wa raia wa Ufaransa na maslahi ya Paris kuhujumiwa. Licha ya
kuweko vitisho hivyo na manung'uniko ya wananchi pamoja na vyama vya
kisiasa vya Ufaransa dhidi ya hatua ya Paris ya kuingia kijeshi nchini
Mali, lakini Rais Francois Hollande ametia pamba masikioni na kutangaza
wazi kuunga mkono kutumwa majeshi ya nchi hiyo kaskazini mwa Mali. Hatua
ya Ufaransa ya kuingia kijeshi inaonekana haijapata himaya ya kila
upande barani Ulaya. Msemaji wa Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya
amesema kuwa, umoja huo hauna nia ya kuingia kijeshi huko Mali bali
utatuma tu wanajeshi wa kutoa mafunzo kwa vikosi vya Bamako. Mjumbe na
mwakilishi wa Russia katika masuala ya Afrika ametangaza kuwa,
operesheni yoyote ile ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Mali inapaswa
kuidhinishwa na kupasisha na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. Ndani
ya Ufaransa mambo si shwari kwani sauti za ukosoaji hatua ya jeshi la
nchi hiyo kuingia kijeshi huko Mali zinazidi kuongeza. Viongozi wa chama
cha mrengo wa kulia nchini humo wanasema kuwa, Rais Hollande amefanya
kosa kuingia kijeshi huko Mali bila ya kushauriana na Bunge pamoja na
Baraza la Mawaziri. Dominique de Villepin, Waziri Mkuu wa zamani wa
Ufaransa naye amejitokeza na kuikosoa hatua hiyo ya Rais Holllande na
kusisitiza kwamba, haikuwa sahihi. Kukithiri malalamiko na ukosoaji huo
kumewafanya Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Waziri wa Ulinzi Laurent
Fabius na Jean- Yves le Drian kwenda katika kikao cha baraza la taifa la
nchi hiyo, kilichoitishwa kwa lengo la kujadili uingiaji kijeshi wa
Paris huko Mali na uhalali wa hatua hiyo. Licha ya kuwa viongozi wa
Ufaransa wanadai hatua yao hiyo ni ya kibinadamu yenye lengo la kuunga
mkono mamlaka ya kujitawala Mali, lakini weledi wa mambo wanaamini
kwamba, lengo kuu la Paris kuingia kijeshi katika nchi hiyo ya Magharibi
mwa Afrika ni kudhibiti vyanzo vya utajiri vya nchi hiyo.